Matthew 27

Isa Aletwa Mbele Ya Pilato

(Marko 15:1; Luka 23:1-2; Yohana 18:28-32)

1 aAsubuhi na mapema, viongozi wa makuhani wote na wazee wa watu wakafanya shauri pamoja dhidi ya Isa ili kumuua. 2 bWakamfunga, wakampeleka na kumkabidhi kwa Pilato, ambaye alikuwa mtawala wa Kirumi.

Yuda Ajinyonga

(Matendo 1:18-19)

3 cYuda, ambaye alikuwa amemsaliti Isa, alipoona kuwa Isa amehukumiwa, akajuta na akarudisha vile vipande thelathini vya fedha alivyopewa na viongozi wa makuhani na wazee wa watu. 4 dAkasema, “Nimetenda dhambi, kwa maana nimeisaliti damu isiyo na hatia.”

Wakamjibu, “Hilo latuhusu nini sisi? Ni shauri yako.”

5 eBasi Yuda akavitupa vile vipande vya fedha ndani ya Hekalu akaondoka akaenda kujinyonga.

6 fWale viongozi wa makuhani wakazichukua zile fedha wakasema, “Si halali kuchanganya fedha hizi na sadaka kwa sababu hizi ni fedha zenye damu.” 7Kwa hiyo baada ya kushauriana, waliamua kuzitumia kununulia shamba la mfinyanzi, liwe mahali pa kuzikia wageni. 8 gHii ndiyo sababu lile shamba likaitwa Shamba la Damu hadi leo. 9 hNdipo likatimia lile lililonenwa na nabii Yeremia, kwamba, “Walichukua vile vipande thelathini vya fedha, thamani aliyopangiwa na watu wa Israeli, 10 iwakanunulia shamba la mfinyanzi, kama vile Bwana alivyoniagiza.”

Isa Mbele Ya Pilato

(Marko 15:2-15; Luka 23:3-25; Yohana 18:33–19:16)

11 jWakati huo Isa akiwa amesimama mbele ya mtawala, mtawala akamuuliza, “Wewe ndiye mfalme wa Wayahudi?”

Isa akasema, “Wewe wasema hivyo.”

12 kLakini viongozi wa makuhani na wazee walipomshtaki, hakujibu neno. 13 lNdipo Pilato akamuuliza, “Je, husikii ni mambo mangapi wanayokushtaki nayo?” 14 mLakini Isa hakumjibu hata kwa shtaka moja, kiasi kwamba mtawala alishangaa sana.

15 nBasi ilikuwa ni desturi ya mtawala kumfungua mfungwa mmoja aliyechaguliwa na umati wa watu wakati wa sikukuu. 16Wakati huo alikuwepo mfungwa mmoja mwenye sifa mbaya, aliyeitwa Baraba. 17 oHivyo umati wa watu walipokusanyika, Pilato akawauliza, “Mnataka niwafungulie nani, Baraba au Isa yeye aitwaye Al-Masihi?” 18 pKwa kuwa alitambua Isa alikuwa amekabidhiwa kwake kwa ajili ya wivu.

19 qPilato akiwa ameketi kwenye kiti cha hukumu, mkewe akampelekea ujumbe huu: “Usiwe na jambo lolote juu ya mtu huyu asiye na hatia, kwa kuwa leo nimeteseka sana katika ndoto kwa sababu yake.”

20 rLakini viongozi wa makuhani na wazee wakaushawishi ule umati wa watu kwamba waombe Baraba afunguliwe, naye Isa auawe.

21Mtawala akawauliza tena, “Ni yupi kati ya hawa wawili mnayetaka niwafungulie?”

Wakajibu, “Baraba.”

22 sPilato akawaambia, “Basi nifanye nini na huyu Isa aitwaye Al-Masihi?”

Wakajibu wote, “Msulubishe!”

23Pilato akauliza, “Kwa nini? Amefanya kosa gani?”

Lakini wao wakazidi kupiga kelele, wakisema, “Msulubishe!”

24 tPilato alipoona kwamba hawezi kufanya lolote, lakini badala yake ghasia zilikuwa zinaanza, akachukua maji, akanawa mikono yake mbele ya ule umati wa watu, akasema, “Sina hatia juu ya damu ya mtu huyu, hili ni jukumu lenu!”

25 uWatu wote wakajibu, “Damu yake na iwe juu yetu na juu ya watoto wetu!”

26 vBasi akawafungulia Baraba. Lakini baada ya kuamuru Isa achapwe mijeledi, akamtoa ili asulubishwe.

Askari Wamdhihaki Isa

(Marko 15:16-20; Yohana 19:2-3)

27 wKisha askari wa mtawala wakampeleka Isa kwenye Praitorio
Praitorio maana yake ni makao makuu ya mtawala, jumba la kifalme lililokuwa linakaliwa na Pontio Pilato huko Yerusalemu, palipokuwa na kiti cha hukumu.
na wakakusanya kikosi kizima cha askari kumzunguka.
28 yWakamvua nguo zake na kumvika vazi la rangi nyekundu, kisha 29 zwakasokota taji ya miiba, wakaiweka kichwani pake. Wakamwekea fimbo katika mkono wake wa kuume, na wakapiga magoti mbele zake na kumdhihaki, wakisema, “Salamu, mfalme wa Wayahudi!” 30 aaWakamtemea mate, wakachukua ile fimbo wakampiga kichwani tena na tena. 31 abBaada ya kumdhihaki, wakamvua lile joho, wakamvika tena nguo zake. Kisha wakampeleka ili wakamsulubishe.

Isa Asulubishwa

(Marko 15:21-32; Luka 23:26-43; Yohana 19:17-27)

32 acWalipokuwa wakienda, wakakutana na mtu mmoja kutoka Kirene, jina lake Simoni, nao wakamlazimisha kuubeba ule msalaba. 33 adWakafika mahali palipoitwa Golgotha (maana yake ni Mahali pa Fuvu la Kichwa). 34 aeHapo wakampa Isa divai iliyochanganywa na nyongo ili anywe; lakini alipoionja, akakataa kuinywa. 35 afWalipokwisha kumsulubisha wakagawana mavazi yake kwa kuyapigia kura. [Hili lilifanyika ili litimie lile neno lililonenwa na nabii, “Waligawa nguo zangu miongoni mwao na vazi langu wakalipigia kura.”] 36 agKisha wakaketi, wakamchunga. 37 ahJuu ya kichwa chake, kwenye msalaba, wakaandika shtaka lake hivi: Huyu ni Isa, Mfalme wa Wayahudi. 38 aiWanyang’anyi wawili walisulubiwa pamoja naye, mmoja upande wake wa kuume na mwingine upande wa kushoto. 39 ajWatu waliokuwa wakipita njiani wakamtukana huku wakitikisa vichwa vyao 40 akna kusema, “Wewe ambaye utalivunja Hekalu na kulijenga kwa siku tatu, jiokoe mwenyewe basi! Kama wewe ni Mwana wa Mungu, shuka kutoka msalabani.”

41Vivyo hivyo, viongozi wa makuhani, walimu wa sheria pamoja na wazee wakamdhihaki wakisema, 42 al“Aliwaokoa wengine, lakini hawezi kujiokoa mwenyewe! Yeye ni Mfalme wa Israeli! Ashuke sasa kutoka msalabani, nasi tutamwamini. 43 amAnamwamini Mungu, basi Mungu na amwokoe sasa kama anamtaka, kwa maana alisema, ‘Mimi ni Mwana wa Mungu.’ ” 44 anHata wale wanyang’anyi waliosulubiwa pamoja naye wakamtukana vivyo hivyo.

Kifo Cha Isa

(Marko 15:33-41; Luka 23:44-49; Yohana 19:28-30)

45 aoTangu saa sita hadi saa tisa giza liliifunika nchi yote. 46 apIlipofika saa tisa, Isa akapaza sauti akalia, “Eloi, Eloi, lama sabakthani?” Maana yake, “Mungu wangu, Mungu wangu, mbona umeniacha?”

47Baadhi ya watu waliokuwa wamesimama pale waliposikia hayo, wakasema, “Anamwita Ilya.”

48 aqGhafula mmoja wao akaenda mbio na kuleta sifongo, akaichovya kwenye siki, akaiweka kwenye mwanzi na akampa Isa ili anywe. 49Wengine wakasema, “Basi mwacheni. Hebu tuone kama Ilya atakuja kumwokoa.”

50 arIsa alipolia tena kwa sauti kuu, akaitoa roho yake.

51 asWakati huo huo pazia la Hekalu likachanika vipande viwili, kuanzia juu hadi chini. Dunia ikatetemeka na miamba ikapasuka. 52Makaburi yakafunguka na miili ya watakatifu waliokuwa wamekufa ikafufuliwa. 53 atWakatoka makaburini, na baada ya Isa kufufuka, waliingia kwenye Mji Mtakatifu na kuwatokea watu wengi.

54 auBasi yule jemadari na wale waliokuwa pamoja naye wakimlinda Isa walipoona lile tetemeko na yale yote yaliyokuwa yametukia, waliogopa, wakasema, “Hakika huyu alikuwa Mwana wa Mungu!”

55 avWalikuwako wanawake huko wakiangalia kwa mbali. Hawa walikuwa wamemfuata Isa tangu Galilaya ili kushughulikia mahitaji yake. 56 awMiongoni mwao walikuwepo Maria Magdalene, na Maria mama yao Yakobo na Yusufu, na mama yao wana wa Zebedayo.

Maziko Ya Isa

(Marko 15:42-47; Luka 23:50-56; Yohana 19:38-42)

57 axIlipofika jioni, alifika mtu mmoja tajiri kutoka Arimathaya aitwaye Yusufu, ambaye pia alikuwa mwanafunzi wa Isa. 58Akamwendea Pilato ili kumwomba mwili wa Isa. Pilato akaamuru apewe. 59Yusufu akauchukua mwili wa Isa, akaufunga katika kitambaa cha kitani safi, 60 ayna kuuweka katika kaburi lake mwenyewe jipya, alilokuwa amelichonga kwenye mwamba. Kisha akavingirisha jiwe kubwa katika ingilio la kaburi, akaenda zake. 61Maria Magdalene na yule Maria mwingine walikuwepo mahali pale, wakiwa wameketi mkabala na kaburi.

Walinzi Pale Kaburini

62Kesho yake, yaani siku iliyofuata ile ya Maandalizi ya Sabato, viongozi wa makuhani na Mafarisayo wakamwendea Pilato 63 azna kusema, “Bwana, tumekumbuka kwamba yule mdanganyifu wakati alikuwa bado hai alisema, ‘Baada ya siku tatu nitafufuka.’ 64 baKwa hiyo uamuru kaburi lilindwe kwa uthabiti mpaka baada ya siku tatu. La sivyo, wanafunzi wake wanaweza kuja kuuiba mwili wake na kuwaambia watu kwamba amefufuliwa kutoka kwa wafu. Udanganyifu huu wa mwisho utakuwa mbaya kuliko ule wa kwanza.”

65 bbPilato akawaambia, “Ninyi mnao askari walinzi. Nendeni, liwekeeni ulinzi kadri mwezavyo.” 66 bcKwa hiyo wakaenda na walinzi ili kulilinda kaburi kwa uthabiti, wakatia muhuri kwenye lile jiwe na kuweka ulinzi.
Copyright information for SwhKC